KATIKA kuboresha huduma ya usafiri wa teksi mkoani Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda amewataka madereva wa usafiri huo kuhakikisha wanakaa na kujadili mfumo bora wa uendeshaji wa biashara zao kwa manufaa yao na abiria.
Makonda alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na madereva teksi wa mkoa huo ili kuzungumza namna bora ya kuboresha huduma hiyo na kuwa ya tofauti.
“Nawapa wiki moja mkae mjadiliane na mkija hapa mje na majibu ya kutatua kero zenu pamoja na namna bora ya kuendesha biashara zenu bila bugudha,” alisema Makonda.
Alisema katika kuboresha huduma hiyo ni lazima kiwepo mfumo mzuri ambao utakuwa na manufaa kwa madereva hao pamoja na watumiaji hivyo anataka mfumo wa ukadiriaji wa gharama za usafiri wa teksi uondoke katika mkoa huo na abiria wasikadiriwe gharama badala yake anapaswa kujua gharama
. “Azma ya Serikali ni kuboresha huduma za usafiri na kuwa wa kipekee ili kukamilisha hilo nataka teksi zote kuanza kutumia vifaa maalumu vitakavyoonesha umbali wa eneo analokwenda abiria kuondoa gharama za ukadiriaji kwani kwa kufanya hivyo kutaisaidia Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwatoza kodi stahiki kulingana na magari yenu,” alisema Makonda.
Aidha Makonda alisema serikali yake imejipanga kuziondoa teksi bubu zote, na utaratibu wa kuweka rangi na namba kwenye magari utarudi ili magari yatambulike.
“Tutaziondoa teksi bubu zote na yeyote atakayetumia akumbuke akikumbwa na tatizo hakuna atakayemsaidia, tutaendeleza mfumo wa kupaka rangi na kutoa namba kwa teksi zote ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora, “ aliongeza.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa madereva wa teksi Ilala, Jacob Anyandwile, alimuelezea Makonda changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na kutozwa kodi kubwa na TRA pamoja na uwepo wa huduma ya teksi kwa njia ya mtandao unafanywa na kampuni ya UBA aliyodai pia kuwa wanatumia pia teksi bubu jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment