• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Friday, December 26, 2014


Thursday, December 25, 2014


Katika ulimwengu wa vyakula, inafahamika na kuaminika kuwa chakula ni dawa. Chakula unachokula leo ndicho kinachoamua hali yako ya kiafya kesho. Unaweza kuishi bila kuugua kama ukila vyakula vyote muhimu vinavyohitajika mwilini.

Leo nitakutajia orodha ya juisi zilizotengenezwa kwa matunda na mboga na fadia zake mwilini. Katika orodha hii, utaona kuna mchanganyiko wa matunda au mboga mbili hadi nne na kazi zake mwilini, zikitumika kama tiba au kinga ya magonjwa.

KAROTI, TANGAWIZI NA TUFAHA
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda hayo matatu huondoa sumu mwilini na kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili. Tufaha ndiyo apple kwa Kiingereza.

TUFAHA, TANGO NA FIGILI
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya ni kinga dhidi ya saratani, huondoa lehemu (cholestrol) mwilini, husafisha tumbo na pia huondoa maumivu ya kichwa.

NYANYA, KAROTI NA TUFAHA
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya hufanya ngozi ya mwili mzima kuwa nyororo na huondoa harufu mbaya mdomoni.

TUFAHA NA TANGO LA KAWAIDA
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya huondoa harufu mbaya mdomoni na hupunguza joto la mwili.

CHUNGWA, TANGAWIZI NA TANGO
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya hung’arisha rangi ya ngozi na kuifanya kuwa laini. Pia hupunguza joto la mwili. Kwa wale wenye matatizo ya kuwa na ngozi kavu, juisi hii itawasaidia sana.

NANASI, TUFAHA NA TIKITIMAJI
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya hufanya kazi ya kuondoa chumvi nyingi mwilini, husafisha kibofu cha mkojo na figo. Juisi hii ni nzuri kwa wale wenye matatizo ya kibofu na figo au wanaotaka kujikinga na magonjwa hayo.

TUFAHA, TANGO NA ‘KIWI’
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya hung’arisha rangi ya ngozi. Kiwi ni aina ya matunda ambayo hujulikana pia kama ‘matunda-damu’.

PEASI NA NDIZI

Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya hurekebisha kiwango cha sukari katika damu. Inawafaa sana wagonjwa wa kisukari na inaweza kuwa sawa na kinga dhidi ya ugonjwa huo.

KAROTI, PEASI, TUFAHA NA EMBE
Juisi yenye mchanganyiko wa matunda haya huzuia athari ya sumu mwilini, hupunguza shinikizo la damu na kuondoa mlundikano wa uchafu mwilini.

MASEGA YA ASALI, ZABIBU, TIKITIMAJI NA MAZIWA
Juisi yenye mchanganyiko huu huwa na kiasi kikubwa cha Vitamin C na Vitamin B2 ambazo huimarisha chembechembe hai na kinga ya mwili.

PAPAI, NANASI NA MAZIWA
Juisi hii ina kiwango kikubwa cha Vitamin C, E na madini chuma. Huimarisha rangi ya ngozi na mfumo wa usagaji wa chakula tumboni.

NDIZI, NANASI NA MAZIWA 
Juisi hii yenye kiasi kikubwa cha vitamini na virutubisho mbalimbali vyenye faida mwilini, huzuia tatizo la ukosefu wa choo.

Ili kupata faida hizo zilizoainishwa katika kundi la matunda hayo, usafi wa matunda yenyewe hauna budi kuzingatiwa wakati wa kutayarisha juisi yake. Vilevile hakikisha unatumia matunda yaliyoiva vizuri na uyatayarishe kwa kuzingatia kanuni ya ‘mtu ni afya’.

Unaweza kutumia mashine maalumu ya kukamulia matunda (blender) au kutumia njia ya asili ya kutwanga kwa kinu maalumu na kupata juisi hiyo. Kama utaongeza sukari, inashauriwa kuweka kiasi kidogo sana. Ni bora zaidi usipoweka sukari, kwa sababu matunda mengi yana sukari ya asili.


Papai na Parachichi-2-pic by F Macha
Imekuwa kazi sana kupiga picha ya mseto huu mzuri na mtamu leo kabla ya kuushughulikia.
Afrika imejaaliwa mimea, madini, rutuba na hali ya hewa safi.
Takribani vyakula vyote tunavyohitaji wanadamu hupatikana bara hili. Lakini pamoja na hayo uhai wetu mfupi kuzidi wengine duniani. Kufuatana na orodha ya wastani wa maisha iliyotolewa na shirika la Ujasusi Marekani (CIA)na Umoja wa Mataifa mwaka 2011- nchi zinazoongoza kwa maisha marefu ni Japani na chini kabisa ni Afrika.
Machenza na Nanasi
Wajapani wanaishi hadi miaka 90 kuendelea , Ulaya, Marekani na China kati ya 75 hadi 90; nchi za bara Asia (mathalan India) miaka 65 kuendelea; mwisho ni Afrika yenye taifa la Angola mkiani (miaka 40). Tanzania imewekwa na wastani wa miaka 50 hadi 53.
Kombu la Kijapani
Msingi wa sababu zinazowafanya watu wasiishi muda mrefu ni maendeleo ya uchumi-jamii na siasa.
Lakini kiini cha wewe kuishi (mbali na elimu, makazi bora na furaha moyoni )ni CHAKULA BORA NA NAMNA UNAVYOKILA.

Wajapani mathalan wanasifika kwa kula vyema- hawali misosi mikubwa mikubwa kama sisi. Ulaji wao ni mdogo mdogo, wa mara kwa mara- hawajazi sana matumbo. Halafu kuna vitu wanavyokula ambavyo husaidia sana kukarabati na kuhifadhi mwili. Mfano mzuri ni mimea ya baharini. Kuna mmea uitwao Kombu ambao unauchemsha na kuyatumia maji yake kwa kupikia mchuzi, chai, nk. Moja ya faida ya “Kombu” ni kukinga na kuuponyesha mwili kutokana na maradhi; pili, kuongeza nguvu za nywele, ngozi na maisha kijumla. Ndiyo maana nadra sana kumwona Mjapani asiyekua na nywele nyingi, hata akiwa mzee- huwaoni wana mvi. Mvi ni dalili ya ukosefu wa madini mwilini.
Wana afya.
Pumpkin Seeds
Mbegu mbichi kama hizi za Maboga zina faida kubwa sana mwilini : mafuta asilia yasiyodhuru moyo-kama nyama, kinga maradhi, ujenzi na kukarabati ngozi, mifupa, kucha, nywele, kuupa mwili nguvu za rijali nk.
Wenzetu nchi zilizoendelea wanathamini sana matunda na mboga mboga. Si ajabu leo wanaishi maisha marefu kutuzidi.
Sisi tumevijaza vyote hivi, TELE, lakini hatuvithamini.
Zamani nikiwa mtoto ilikuwa kawaida mapishi kuwa na mboga za majani na saladi (kachumbari) leo kutokana na kuingizwa kwa utamaduni wa “vyakula vya haraka “ (“junk”) na “ladha” –vyenye CHUMVI NA MAFUTA MAFUTA MENGI YA KUKAANGA kama chips, nyama choma nk, hatuli sana mboga mbichi mbichi za majani. Na zikipikwa zinachemshwa hadi zinageuka nyani.
Steamed Broccoli-F Macha
Mchanganyiko wa matango na brokoli, nilioutayarisha kwa “mvuke” – yaani kubandika sufuria yenye hizo mboga juu ya nyingine inayochemka chini yake. Upishi huu “barabara” hufanya mboga zisiunguzwe au kuiva sana- zinabakia imara.
Steaming pan-1
Steaming pans
WANGAPI TUNAKULA MATUNDA KWA WINGI AFRIKA?
Kiafya unatakiwa ule matunda aina tano kwa siku kupata faida zake zote mwilini.
Faida za matunda hazihesabaki. Na hayatakiwi yaliwe pamoja na chakula- bali kabla- AU KATI KATI YA MILO MIKUBWA. baadaye. Tabia yetu wengi kuchanganya matunda na milo mikubwa kama wali, ugali, chapati na kadhalika – hausaidii – ni afadhali hata usile kabisa.
Ndizi Mbivu
Matunda humeng’enywa kwa vimeng’enyo tofauti na vyakula mama (wanga, protini, nk). Kati ya faida kuu za matunda ni:
1. Zuia maradhi , rutubisha na kinga mwili
2. Sukari , nguvu na mafuta asilia
3. Madini na Vitamin mbalimbali yanayosaidia kujenga, kukarabati na hata kuzuia bakteria na maadui wakubwa wakubwa wa miili yetu mathalan “free radicals”- tunaweza kulinganisha “free radicals” na majivu yanayobakia baada ya moto kuwaka. Hutolewa mwilini kama taka au kuingia mwilini kutokana na uchafu wa mazingira, mioshi ya sigara na magari, taka taka za mashine za kisasa – tena siku hizi wengi tunalala na simu za mkononi zikiwa zimewashwa, tunazibeba kwa wingi. Taka au majivu haya ndiyo kiini kikuu cha maradhi ya kisasa (nchi zilizoendelea) mathalan saratani.
Chenza
 MACHUNGWA
Ndizi Kisukari-pic by F Macha
NDIZI
Maparachichi Mawili-by F Macha
 MAPARACHICHI
Tikiti Maji-1
 TIKITI MAJI
Cherries
Mcheri…tunda lenye faida nyingi ikiwemo kusaidia maradhi ya Jongo.
Cherry ambalo hupendwa sana na ndege, lina faida nyingi sana miongoni kusaidia kupambana na maradhi yanayosakama damu au mzungunguko wa maji mwilini kama Jongo. Jongo ni ugonjwa unatokana na aidha kurithi, kunywa sana pombe, nyama nyekundu, mayai, kutofanya mazoezi. Hujionyesha kwa maumivu makali katika goti moja au kidole gumba cha mguu. Cherry safi sana.
Strawberry-Apricot

Strawberries
Stroberi (Strawberry) – tunda linalopatikana zadi Uzunguni- ambalo lina Vitamin C kwa wingi.
 Acids-Mango Oranges Kiwi
Matunda chachu (“asidi”) yanatakiwa yaliwe pamoja…
Mapapai na Maparachichi yanaangukia katika mkondo wa “alkali” na moja ya matunda yaliyowekwa katika Vyakula Vyenye Nguvu kuliko vyote (Superfoods) . Matunda hayo ni Machungwa , Kiwi, Papai, Parachichi. Vyakula hivi via faida sana mwilini.
Alkalines-Apples Pears Ndizi-FMacha
Mfano wa matunda yenye “alkali” yanayotakiwa kuliwa pamoja.
Faida zake ni zifuatazo.
1. Kinga maradhi na kinga magonjwa (Anti-Oxidant) ambazo husaidia kukinga na kupambana na takataka zinazotolewa na mwili au zinazotoka katika mazingira machafu.
2. Vitamin C. Vitamin hii ni muhimu sana mwilini. Ukosefu wa Vitamin C husababisha uchovu, kukosa usingizi, uvivu, kutokuwa na hamu ya kula. Kwa siku mtu mzima unatakiwa upate gramu 40 za Vitamin C. Kwa wavuta sigara zidisha mara mbili. Ukila matunda yenye Vitamin C unapata kinga ya majeraha mwilini (vidonda pona haraka), huboresha wajihi, haiba na “nafsi” ya ngozi, mifupa, meno na mzunguko mzima wa damu mwilini- hivyo kusaidia usingizi ( na kwa watoto kusaidia kukua vizuri).
Papai-1-pic by F Macha
3. Papai lina “papain” inayosaidia kuukinga mwili na kulainisha tumbo- ndiyo maana kama umevimbiwa au huendi haja kubwa sawasawa (“constipation”) ukila papai husaidia sana.
4. Mapapai na Maparachichi yana “Beta Carotene”(itokanayo na Vitamin A) inayopatikana pia katika nyanya, karote, maembe, mchicha (ambao haukupikwa hadi ukanyong’onyea), mbegu mbegu (mbichi si za kukaanga au kuwekwa chumvi- hadi zikakongoroka) kama hizi pichani chini karanga, mlozi, korosho, nk.
Mseto wa Mbegu Mbichi
Faida zake ni pamoja na kusaidia mizunguko ya umajimaji na damu mwilini, ngozi na nywele (safi sana kwa kina dada wanaojipenda), kupunguza mafuta katika damu (cholestoral) na “presha” – mambo yanayoua sana watu weusi duniani leo. Ukiwa upungufu wa “Beta Karotene” macho hayaoni vizuri, unaugua upesi upesi hasa maradhi ya mapafu (mafua, kikohozi,nk). Kwa wanawake waja wazito ni rahisi kupoteza watoto au kuzaa watoto ambao hawako sawasawa.
5. Maparachichi yanayo mafuta asilia. Mafuta haya ni mazuri SANA kuliko yale tunayoyapata katika nyama au vitu vilivyokaangwa, maana yanausaidia na haya haribu mwili. Makisio yake ni kalori 400 kwa parachichi moja. Hiyo ni nguvu kubwa sana. Ndiyo maana Parachichi (na Papai) huhesabiwa kama mfalme wa matunda.
Papai na Parachichi -nje
Lazima izingatiwe kuwa chakula, mmea au tunda lolote lenye rangi nzito iliyokolea kama parachichi huwa na faida MARIDHAWA mwilini.
Hivyo, kuanzia leo kama hukua ukithamini matunda haya mawili- kayatafute. Kuna watu wazima wanaosema eti matunda ni chakula cha watoto. Wanakosea. Mtu mzima anahitaji kuendelea kuukarabati mwili wake. Kwetu Afrika ni ya bei nafuu- wapo wengi wanaofika Ulaya na Marekani wanashindwa kuyala shauri bei yake si mchezo. Halafu wala si matamu kama ya nyumbani Afrika…

Sunday, December 21, 2014




Sunday, December 14, 2014



Monday, December 1, 2014


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ