• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Thursday, September 18, 2014

Sababu za kumuondoa msimamizi wa mirathi

No comments:
 
Katika jamii kuna tatizo kubwa sana kuhusu mirathi hasa pale mzazi mmoja anapofariki na kuacha mali pasipo na wosia,hivyo mzazi anayebaki na watoto wanaweza kupata taabu kama hakutakuwa na uangalizi wa awali katika kukwepa matatizo yanayoweza kutokea..
Mirathi kwa ujumla ni mali zilizoachwa na marehemu ambazo zinatakiwa zisimamiwe ili warithi waweze kuzifaidi.Kisheria Mirathi ni utaratibu mzima wa kusimamia mali zilizoachwa na marehemu.
Matatizo na ugumu katika familia hutokea pale ambapo marehemu hajaacha wosia kwa watu wanaostahili kurithi mali zake.Watu wanotakiwa kurithi mali za marehemu ni mke,watoto au mtu yeyote aliyekuwa chini ya malezi ya marehemu vilevile sheria imeongeza kuwa hata wazazi wa pande zote mbili au mtu yeyote aliyeahidiwa kurithishwa mali hizo anastahili kupewa.
Msimamizi wa mirathi anaweza kuteuliwa na ukoo kwa kukaa pamoja endapo marehemu hakuteua msimamizi au hata kama ameshateuliwa na marehemu anatakiwa kwenda mahakamani ili atambulike na kuidhinishwa na mahakama asimamie mirathi hiyo kihalali.
Msimamizi huyo anawajibu wa kukusanya mali zote za marehemu,asimamie mali hizo zisiharibiwe kwa njia yoyote ile kama kuiba,kuuzwa au kutumiwa hovyo,pia anatakiwa kulipa madeni ya marehemu na kugawa mirathi kwenda kwa warithi halali
Vilevile katika kusikiliza kesi za mirathi wale wote waliohudhuria katika kikao cha kumteua msimamizi wa mirathi wanatakiwa kufika mahakamani kuthibitisha kuwa wameridhia kuwa na msimamizi huyo......

LEO tutaangalia wajibu wa wasimamizi wa mirathi. Nitazungumzia juu ya usimamizi wa mirathi  pamoja na mambo muhimu  juu ya wanaonufaika na mirathi.
Katika Mahakama za Mwanzo pamoja na  zile mahakama  za juu kuna migogoro mingi inayohusu mirathi, kumpinga msimamizi wa mirathi au mashauri ambayo mara kwa mara hufunguliwa na ndugu wa marehemu wakimtuhumu msimamizi kufuja mali za marehemu.
Sheria ya usimamizi wa mirathi sura ya 352 ya sheria za Tanzania, ndiyo nitakayoirejea katika kuzungumzia wajibu wa wasimamizi wa mirathi.
Lengo kuu la sheria hii ni kutoa utaratibu wa kusimamia mali za marehemu baada ya kifo chake, ikiwamo kuhamisha umiliki wa mali hizo kutoka kwa marehemu kwenda kwa watu wenye haki ya kuzipata mali hizo.
Madhumuni hasa ni kwamba mali alizoacha marehemu zisibaki zikiharibika na kupotea bure, au warithi halali au watu wenye masilahi na mali za marehemu, mathalani  wale wanaomdai hawapotezi haki hiyo, bali awepo mtu atayezisimamia na kuzigawa kwa wahusika wakiwamo wadai na kuepusha mgongano katika jamii husika.
Hivyo, sheria inamuweka msimamizi wa kugawa mirathi husika na mamlaka yake.
Kazi ya usimamizi wa mirathi ni kazi inayohitaji uaminifu wa hali ya juu.
Na ni vema ndugu wawe makini hasa  katika kuchagua watu hawa kutokana na madaraka makubwa ambayo sheria inawapa.
Uchaguzi mbaya wa msimamizi wa mirathi unaweza kuleta madhara makubwa kwenye familia nyingi na matokeo yake mali hupotea.
Hebu tuangalie mamlaka ya kisheria aliyonayo msimamizi wa mirathi.
Msimamizi wa mirathi ndiye atakuwa mwakilishi halali wa kisheria wa mambo yote ya marehemu na mali zote za marehemu kisheria zitakuwa chini yake, na naomba ieleweke mali hizo zitakuwa chini yake kama msimamizi na si kwamba ni mali yake (si mmiliki).
Katika kesi ya Mohamed Hassan na Mayasa Mzee dhidi ya Mwanahawa Mzee [1994] T. LR 225 Mahakama ya Rufaa iliamua kwamba kisheria msimamizi wa mirathi hulazimika kupata ruhusa kutoka kwa warithi kabla ya kuuza mali yoyote ya marehemu.
Hata hivyo katika kesi nyingine ya  Aziz Daudi Aziz  dhidi ya Amin Ahmed Ally na Another CIV. App No.30 of 1990 [unreported] , Mahakama ya Rufaa iliamua kwamba pale tu msimamizi wa mirathi anapoteuliwa,mali zote zinakuwa chini ya mamlaka yake kama msimamizi na anachukua majukumu aliyokuwa nayo marehemu kwenye mali yake wakati yu hai.
Msimamizi huyu huachiwa kuamua jinsi ya kushughulikia mirathi hiyo kadiri atakavyoona inafaa.
Kwa upande mwingine, msimamizi atakuwa na mamlaka ya kufungua mashitaka mahakamani kwa niaba ya marehemu au kushitakiwa kwa niaba ya marehemu na atawajibika kulipa madeni ya marehemu kutoka katika mali alizoacha marehemu.
Msimamizi wa mirathi vilevile atakuwa na uwezo wa kuhamisha umiliki wa mali za marehemu kama atakavyoona inafaa kwa kuziweka rehani, kuziuza au kuzikodisha, kwa kuzingatia masilahi ya warithi na watu wanaomdai marehemu.
Hivyo  ni sawa na kusema msimamizi wa mirathi hawezi tu kuamka na kutangaza kuuza mali za marehemu bila sababu za msingi.
Pia atawajibika kutumia kiasi fulani cha pesa za marehemu kwa ajili ya kutunza mali za marehemu ziwe katika hali nzuri na zisiharibike.
Msimamizi wa mirathi anatakiwa ndani ya miezi sita tangu apewe usimamizi au ndani ya muda mahakama ambao itaona unafaa, anatakiwa apeleke mahakamani na kuonyesha mali zote za marehemu na thamani yake halisi.
Madeni yake anayodaiwa au anayodai marehemu na ndani ya mwaka mmoja msimamizi wa mirathi atatakiwa tena kama mahakama itakavyoona inafaa, aonyeshe mali za marehemu zilizo mikononi mwake na jinsi alivyozifanya au kuzishughulikia.
Mahakama ina uwezo wa kuendelea kumuongezea muda mhusika kadiri itakavyoona inafaa.
Lakini kama msimamizi wa mirathi atatakiwa na mahakama kuonyesha mali za marehemu na akashindwa kufanya hivyo ndani ya muda aliopewa, atakuwa ametenda kosa la jinai na akipatikana na hatia atatakiwa alipe faini au apewe kifungo cha miezi sita.
Na kama ataonyesha mali hizo kwa nia ya kudanganya au kuficha atakuwa ametenda kosa la jinai ambalo kifungo chake ni miaka saba.
Mtu yeyote mwenye masilahi na mirathi anao uwezo wa kufanya ukaguzi ili kujiridhisha na usimamizi wa mirathi ya marehemu.
Msimamizi wa mirathi vilevile anatakiwa akusanye mali za marehemu na madeni aliyokuwa akidai na kulipa madeni aliyokuwa akidaiwa.
Katika madeni aliyokuwa anadai marehemu ni vizuri msimamizi wa mirathi akayadai mapema ili yasije yakapitwa na wakati kisheria.
Pamoja na hayo, msimamizi wa mirathi hatakiwi kujipatia faida kutokana na usimamizi wa mirathi hiyo na kama msimamizi wa mirathi mwenyewe au kwa kupitia kwa mtu mwingine atanunua mali ya marehemu, uuzaji huo unaweza kukataliwa kisheria na mtu yeyote mwenye masilahi na mirathi hiyo.
Moja ya sababu ya kufanya hivyo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa akajiuzia mali hizo kwa bei ya chini kuliko thamani halisi ya mali husika.
Vilevile ni jukumu la msimamizi wa mirathi kutoa fedha kwa ajili ya shughuli za mazishi ya marehemu, ila gharama hizo ziangalie hali halisi ya maisha ya marehemu na kama ameacha kiasi cha mali cha kutosha kwa ajili ya shughuli hiyo; na kama msimamizi wa mirathi alitoa fedha yake kwa ajili hiyo, haki ya kwanza ni kulipwa fedha zake kabla ya madeni mengine ya marehemu.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ