Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ambayo imedhamiria kulirejeshea uhai kamili Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya nne, jana imeeleza muda zitakapotua nchini.
Akijibu swali Bungeni, lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Joyce Bitta (Chadema|), kwa niaba ya waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi; Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alisema kuwa ndege hizo zitangia nchini kwa awamu mbili ndani ya miaka miwili ijayo.
Dk. Kalemani alieleza kuwa ndege mbili za mwanzo zenye uwezo wa kubeba abiria 78 kila moja zitatua nchini mwanzoni mwa mwaka ujao (2017), na nyingine mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 120 na 155 zitaingia nchini mwaka 2018.
“Ndege hizo zitaiwezesha ATCL kurejesha safari zake za Johannesburg-Afrika Kusini, Afrika Magharibi, India na Arabuni,” alisema Dk. Kalemani.
Alisema kuwa mbali na ndege hizo, Serikali ina mpango wa kununua ndege nyingine za masafa marefu zitakazokuwa na uwezo wa kwenda katika mabara ya Asia na Ulaya.
No comments:
Post a Comment