• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Wednesday, June 10, 2015

Mkasa uliompata Rais wa Misri nchini Ujerumani

No comments:
 

Kisa cha kushangaza na kufadhaisha kimetokea katikati ya wiki iliyopita katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.
Rais wa Misri, Abd al-Fattah Al-Sisi, alikuwa katika ziara rasmi ya siku tatu ambayo ilizusha mabishano miongoni mwa wanasiasa wa Ujerumani kabla na zaidi wakati ilipokuwa inafanyika.
Wako wale waliosema kwamba licha ya utawala wa Al-Sisi tangu ulipompindua kutoka madarakani na kumtupa gerezani mtangulizi wake, Mohammed Mursi wa Chama cha Udugu wa Kiislamu, umefurutu ada katika kukandamiza haki za binadamu, hata hivyo, ni vizuri kufanya mazungumzo na kiongozi huyo.
Hawa walitoa sababu kuwa Misri ni taifa kubwa la Kiarabu ambalo liko katika eneo tete na lenye ufunguo wa kuyatatua matatizo ya eneo hilo.
Lakini kuna wanasiasa wengine waliohoji kwamba madikteta kama huyo wa Misri- aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi chini ya Mursi, ni mtu anayekanyaga haki za binadamu na kuwafumba midomo maelfu ya wapinzani wake kwa kuwatia magerezani, hivyo hastahiki kupokelewa Ujerumani.
Spika wa Bunge la Ujerumani, Nobert Lammert, alisema hana nafasi ya kukutana na mkuu huyo wa kutoka Mto Nile. Alimlaumu kwa kwenda kinyume na misingi ya demokrasia na kuthubutu hata kumtia gerezani Spika wa Bunge alilolivunja.
Hata hivyo, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauk, alimpokea kwa mazungumzo punde alipowasili, japokuwa mazungumzo yao yanasemekana yalikuwa ya moto. Gauk alimpa mgeni huyo darasa juu ya haki za binadamu na kuheshimu roho za wanadamu.
Japokuwa Serikali ya Ujerumani hapo kabla ilitoa sharti kwamba Kansela Angela Merkel atakuwa tayari tu kukutana na Al-Sisi ikiwa uchaguzi wa Bunge utafanywa huko Misri, hata hivyo, hilo halijatimizwa.
Wakati ulipowadia, Merkel aliamua ni kwa masilahi ya Ujerumani kukutana na mgeni huyo. Misri ina umuhimu wa kijeshi katika eneo lililojaa mizozo, ubavuni mwake ikiwapo Libya ambako huko mifumo ya kidola imesambaratika, na Syria iliyovurugika kutokana na vita vya kienyeji.
Kansela anahisi Misri inaweza kutoa mchango mkubwa katika kupatikana suluhisho la Mashariki ya Kati baina ya Israel na Wapalastina.
Katika mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari, Merkel alitaja kwamba kumekuwako tofauti baina ya misimamo yao. Kwa mfano, Wajerumani hawakubaliani na adhabu ya kifo na inataka kuwapo kwa uhuru kwa dini zote nchini Misri.
Naye Al-Sisi alijinata na kujibu:“ Na sisi tunaishi katika demokrasia na uhuru, lakini tunaishi katika wakati mgumu.“ Alisema hatakubali kuiachia Misri itumbukie katika vita vya kiraia kama vile Syria, Iraq na Yemen, kwa hivyo ataendelea kupambana na wapinzani wake kwa nguvu zake zote.
Pia, alisema analifahamu tatizo la adhabu ya kifo kwa mtizamo wa Ujerumani na Ulaya, lakini wao Wamisri wanauheshimu msimamo huo, lakini wanawatarajia pia Wazungu nao wauheshimu msimamo wao.
Kioja ukumbini
Wakati hayo yanasemwa ghafla alichomoka kijana wa kike aliyevaa mtandio kichwani na kumwonyeshea kidole Al-Sisi na kwa sauti kubwa kumwambia: ‚“ Wewe ni muuaji, wewe ni Nazi na Fashisti.“
Mara katika upande wa pili wa ukumbi wakasimama waandishi wa habari wa Kimisri waliofuatana na rais wao na wao kwa sauti kubwa, huku wakirusha juu mikono kwa hasira, wakajibu: Iishi Misri. Mwanamke huyo alibebwa na kutolewa kwenye ukumbi. Lakini muhimu ujumbe ulifika. Mkuu huyo wa Misri aliaibika na pia mwenyeji wake.
Ukweli ni kwamba ziara hii ya Al-Sisi ilikuja katika wakati wa mashaka kwani siku moja kabla mahakama ya Cairo iliahirisha hadi Juni 16 kutoa uamuzi juu ya hukumu ya kifo iliotolewa dhidi ya rais wa zamani Mohammed Mursi.
Hakimu alisema maoni ya Mufti, mkuu wa juu kabisa wa kidini wa upande wa dola, yaliwasilishwa juu ya hukumu hiyo mwanzoni mwa wiki. Hiyo ni kusema kwamba baada ya Juni 16 uamuzi utatolewa wa kuthibitisha hukumu ya kifo kwa Mursi na wenzake 105.
Mwaka jana pekee, watu 1400 walihukumiwa kifo katika kesi zilizoendeshwa harakaharaka. Wakati mmoja, watu 500 walishtakiwa kwa mkupuo mmoja kwa tuhuma ya kumuua polisi mmoja. Kutokana na hukumu hizo serikali ya Misri inataka kuiambia dunia kwamba nchi hiyo ni tulivu, ikizungukwa na nchi jirani zilizozama katika vita na machafuko.
Kwa hivyo, yaonyesha nchi za Ulaya zinabidi zichague ama utulivu unaotokana na ukandamizaji au kuheshimiwa haki za binadamu za watu wenye siasa kali za Kiislamu.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Austria, Sebastian Kurz, ameshawahi kusema pale alipotembelea Cairo hivi karibuni, kwamba Al-Sisi ni mbadala ulio bora kuliko udugu wa Kiislamu na kwamba utawala wa Misri ni mshirika katika vita dhidi ya ISIS.
Wanasiasa wa Ulaya wanaashiria kwamba ni bora kuendelea kufanya mazungumzo na Al-Sisi ili angalau kuwa na ushawishi hata mdogo, kuhusu hali ya haki za binadamu katika Misri. Lakini swali ni: Je, mkakati huo utasaidia?
Je, watu wachache zaidi watakamatwa, watateswa na watapewa hukumu za vifo? Msimamo wa serikali ya Misri umebakia uleule. Haitaki watu wengine waingilie katika mambo ya ndani ya nchi hiyo na inawataka waheshimu uamuzi wa mahakama za Misri.
Yaonyesha pia kwamba siasa ya Serikali ya Berlin na ya nchi nyingine za Ulaya inajengeka katika msingi wa tukubali kukereketwa na zimwi dogo, yaani utawala wa kijeshi wa Al-Sisi , ili zimwi kubwa, yaani chama cha Udugu wa Kiislamu, kitokomee mbali.
Hiyo hata hivyo, ni siasa isiyoangalia mbali. Ikiwa Chama cha Udugu wa Kiislamu hakitakuwa sehemu ya mfumo wa siasa katika Misri, nani atakuwa mbadala ya wao? Kuna hatari watu hao wataangukia katika siasa kali na matumizi ya nguvu na ule mkondo wa siasa za wastani za Kiislamu utapotea hewani. Nchi za Magharibi zinakariri makosa ya hapo kabla. Zinaziunga mkono tawala kandamizi na kufikiria kwamba tawala hizo zitahakikisha kuwako utulivu na kuwa washirika wa kuaminika dhidi ya wapiganaji wa siasa kali za Kiislamu.
Kwa kufanya hivyo nchi hizo za Magharibi zinakubali kuwatenga Waislamu wenye siasa za wastani ili wasizifikie taasisi za dola, hivyo mwishowe kusababisha misimamo mikali.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ