Mbwana Samatta
SIMBA sasa wamekaa mkao wa kula, kwani mwaka huu ni wa neema kwao. Kwanza watapata mgawo wa asilimia 20 za mauzo ya straika wao wa zamani, Mbwana Samatta ambaye ameuzwa katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji akitokea TP Mazembe, pili wanasubiri kulipwa Dola 300,000 zaidi ya Sh 600 milioni ambazo wanaidai Etoile due Sahel ya Tunisia.
Katika mkataba wa Mazembe walipokuwa wanamnunua mchezaji huyo akitokea Simba uliwataka kuwapa Simba asilimia hizo watakapomuuza klabu nyingine jambo ambalo limetimia na wanatarajia kupokea Sh 349 milioni kutoka kwenye mauzo ya Dola 800,000 ambazo mmiliki wa Mazembe, Moise Katumbi amepewa na Genk huku Samatta akikunja fedha ndefu.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liliiamuru Etoile kuilipa Simba ndani ya siku 60 ambazo zinakaribia kumalizika na Simba wamegoma kulipwa nusu nusu, wanataka pesa yao ilipwe kwa wakati mmoja na Etoile wakishindwa kuilipa Simba watakumbana na adhabu ya kushushwa daraja. Hivyo pesa hizo zikilipwa na zile za Samatta basi tatizo la ukata kwao litapungua.
Etoile walimnunua Emmanuel Okwi lakini hawakulipa hata shilingi na baadaye kuachana naye na Simba kulazimika kufungua kesi hiyo ya madai.
Rais wa Simba, Evans Aveva amesema kuwa kwasasa wanasubiri kupata mgawo wao huo na wamepanga pesa hizo kuzipeleka kwenye ujenzi wa uwanja wao uliopo Bunju B ambao utaanza kujengwa hivi karibuni. Kwa makadirio uwanja wa mazoezi na uzio wa nyavu unaweza kutumia Sh 150 milioni hivyo pesa hiyo itatosha kukamilisha ujenzi huo.
“Tunasubiri meneja wa Samatta arudi maana amekwenda Lubumbashi, ndipo tujue mgawo wetu tunapataje, ila tumepanga kuipeleka pesa hiyo kwenye ujenzi wa uwanja mzuri kabisa, fedha za Okwi bado hawajatulipa tunasubiri, muda waliopewa haujaisha, hatutaki kulipwa nusu tunahitaji fedha,’’ alisema Aveva.
No comments:
Post a Comment