MFANO WA SUMMONS
Summons ndio wito maalum wa mahakama. Mara zote unapofuguliwa mashtaka ( unaposhtakiwa) hasa mashtaka ya madai basi ili uweze kufika mahakamani na kujua mashtaka yanayokukabili yaipasa mahakama kutuma wito maalum ambao kwa jina la kitaalam ndio huitwa “summons”.
1.KWANINI WATU HUKATAA KUPOKEA/KUSAINI WITO HUU.
Mara nyingi wito huu unapotumwa baadhi ya watu hukataa kabisa kuupokea na wengine huupokea lakini hukataa kuusaini. Zipo sababu ambazo huwafanya watu wasipokee wito huu :
( a ) Kwanza ni imani kuwa usipopokea wito basi shauri ulilofunguliwa haliwezi kuendelea.
( b ) Sababu nyingine ni kuamini kuwa ukikataa kupokea wito utakuwa umejitoa katika hatia(liability) ya kutambua chochote kinachoendelea hivyo chochote kilichopo mahakamani kitakuwa hakikuhusu.
( c ) Pia wengine hukataa kupokea wito kwa kuamini kuwa kupokea wito ndio kukubali shitaka na hivyo ni bora kuukataa kwa kuwa kufanya hivyo itakuwa ni kukana shitaka. Tutaona hapa chini kama imani hizo zina ukweli wowote.
2. JE KESI HAIWEZI KUENDELEA KWASABABU UMEKATAA KUPOKEA WITO.?
Jibu ni hapana kukataa kwako kupokea wito hukuzuii shauri lililofunguliwa kuendelea. Na hii ni athari ya kwanza kabisa anayoipata mtu aliyekataa kupokea wito. Mtu anapokataa kupokea wito basi yule aliyetumwa kupeleka wito huo atatakiwa kuapa kuwa alimpelekea fulani wito na akakataa kuupokea.
Baada ya kiapo hicho atarejesha taarifa za kukataa kupokelewa kwa wito huo mbele ya hakimu/jaji husika aliyepangiwa kesi hiyo. Sambamba na hilo ataambatanisha kiapo chake kuonesha kukataliwa kupokelewa wito huo. Baada ya hakimu/jaji husika kupokea taarifa hizo basi ataamuru shauri kuendelea upande mmoja(kama ataona inafaa).
Shauri kuendelea upande mmoja maana yake ni kuwa shauri litaendelea bila uwepo wa yule aliyekataa kupokea wito.
Kwa hiyo jibu la swali hili ni kuwa kukataa kupokea au kusaini wito hakuzuii kesi kuendelea.
3. JE KUPOKEA /KUSAINI WITO NI KUKUBALI SHITAKA ?.
Hapana siyo kweli hata kidogo. Unapokubali kupokea wito au kuusaini haimaanishi kwa namna yoyote kuwa umekubali shitaka. Hakuna uhusiano wowote kati ya kupokea/kusaini wito na kukubali mashtaka. Kupokea/kusaini wito maana yake ni kuthibitisha tu kuwa umeona kuwa unaitwa.
Masuala ya kukubali kosa au kukataa yapo mahakamani . Ni pale unapokuwa mahakamani au wakati wa kujibu mashtaka kwa maandishi ndipo unapoweza kukubali au kukataa kosa. Kwahiyo hakuna haja ya kukataa kupokea/kusaini wito kwasababu hiyo.
4. MADHARA YA KUKATAA KUPOKEA/KUSAINI WITO.
( a ) Athari ya kwanza kabisa ni kuendelea kesi bila kuwepo kwa aliyekataa kupokea wito. Kuendelea kwa kesi upande mmoja ni kupatikana kwa hukumu ya upande mmoja.
Na mara nyingi hukumu za upande mmoja ni lazima tu aliyekataa kufika mahakamani awe ameshindwa. Kwahiyo madhara makubwa kabisa yanayopatikana ni kushindwa kesi na kupoteza kabisa hata kile kidogo ambacho alitakiwa kukipata.
Sio rahisi kesi ikasikilizwa upande mmoja halafu aliyesikilizwa akashindwa. Bali ambaye hakufika mahakamani ndiye atakayekuwa ameshindwa.
( b ) Madhara mengine makubwa ni kukosa kusikilizwa. Unapokataa kupokea wito/kuusaini maana yake ni kuwa hautofika mahakamani. Usipofika mahakamani maana yake ni kuwa umejinyima haki ya kusikilizwa. Kumbuka uzoefu huonesha kuwa siku zote mpeleka mashtaka huwa ana kawaida ya kusema vitu vingi vya uongo na uzushi dhidi ya mshitakiwa.
Unaposhindwa kupokea wito na hivyo kutofika mahakamani basi hakuna mtu wa kufika na kukana uongo na uzushi kwa niaba yako. Utaifanya mahakama na umma kuamini kila kinachosemwa na utakuwa umekosa nafasi ya kupinga na kuonesha kusingiziwa.
( c ) Pia upo katika hatari ya kupoteza mali ikiwa mlalamikaji aliyefungua kesi anadai kitu kutoka kwako. Ikiwa anadai mali kama ardhi,nyumba, gari, baiskeli, mifugo, na mali nyingine yoyote basi upo katika hati hati ya kupoteza hata kama ilikuwa ni haki yako.
Hii ni kwakuwa haukufika mahakamani na hivyo umetoa nafasi ya ushindi kwa mlalamikaji ambaye katika kukaza hukumu(execution) ataomba kupatiwa ile mali na mahakama itamteua dalali wa kuhakikisha unakunyanganya ile mali na atakabidhiwa mlalamikaji/mshitaki.
No comments:
Post a Comment