Katika hatua ambayo inahofiwa huenda ikazusha ghasia na machafuko nchini Congo DRC, mfanyabiashara maarufu, Moise Katumbi, ambaye mwezi Mei alitangaza kuwa mgombea urais, amehukumiwa kwenda jela kwa miezi 36 (miaka 3).
Kwa mujibu wa BBC, Moise Katumbi, gavana wa zamani wa Jimbo La Katanga na mmiliki wa timu maarufu ya soka ya TP Mazembe na mwenye umri wa miaka 51 amehukumiwa bila mwenyewe kuwepo mahakamani kwa kosa la kuuza mali isiyohamishika(nyumba) kinyume cha sheria huko Lubumbashi. Hukumu hii ina maanisha Katumbi hatoweza kugombea Urais mwezi Novemba. Katiba ya Congo DRC inakataza mtu yeyote ambaye aliwahi kupatikana na hatia kugombea Urais.
Mbio za urais za Moise Katumbi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, zinaungwa mkono na vyama 7 vya upinzani (maarufu kama G7) kitu ambacho kinasadikika kumkosesha raha Rais wa Congo DRC,Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001. Haijajulikana wazi kama Rais Kabila ataachia madaraka kirahisi baada ya kumaliza muhula wake wa mwisho wa Urais au atafuata nyayo za viongozi wengine barani Afrika kubadili katiba ili aendelee kutawala.
Mbali na adhabu ya kifungo, mahakama ya mjini Lubumbashi pia imempiga faini ya kiasi cha dola milioni $6 kutokana na kosa hilo la kuuza jumba hilo ambalo raia mmoja wa Ugiriki anadai ilikuwa ni mali ya familia yao na yeye angekuwa mrithi wa mali hiyo. Katumbi alituhumiwa kutengeneza makaratasi ya uongo.
Katumbi hakuwepo mahakamani wala nchini kwani aliondoka tangu Mei 20 amri ya kukamatwa kwake ilipotolewa kwa makosa ya kuajiri wageni maadui wa taifa kinyume cha sheria kitu ambacho kinadaiwa alihatarisha usalama wa nchi. Katumbi alikuwa amemuajiri mshauri wa masuala ya kiusalama mmarekani Darryl Lewis, ambaye alikamatwa akiwa na walinzi wengine watatu. Aliachiwa siku sita baadae.
Alifanikiwa kuondoka nchini Congo kwa kisingizio cha kwenda kutibiwa . Baada ya kuondoka alielekea nchini Afrika Kusini kabla ya kwenda London,Uingereza inapoaminika yupo mpaka hivi sasa. Mwenyewe anakana mashtaka yote hayo akiyahusisha na siasa zinazoendelea akidai ni juhudi za Rais Kabila kumzuia asigombee.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza ambalo linamnukuu mwandishi wa AFP inasemekana mwanzo Jaji mmoja miongoni mwa majaji watatu waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo aligoma kutia sahihi hukumu. Katika mshangao wa wengi,masaa machache baada na kabla siku haijamalizika hukumu ilitolewa ikiwa imepigwa sahihi na majaji wote.
Mwanasheria wa Katumbi, Mumba Gama ameiambia AFP kwamba anaamini Jaji huyo amelazimishwa na mamlaka za juu kupiga sahihi kitu ambacho ameridhia kwa shingo upande. Mwanasheria wa Katumbi ameahidi kukata rufaa.
Katumbi na Rais Joseph Kabila walikuwa washirika kwa muda mrefu mpaka mwezi Septemba mwaka jana walipohitilafiana baada ya Rais Kabila kutangaza mpango wake wa kuligawa jimbo la Katanga ambalo ukubwa wake unalinganishwa na nchi ya Hispania katika majimbo mengine manne. Katumbi alipingana na wazo la Rais Kabila na kujiunga na upinzani kwa chama cha People’s Party for Reconstruction and Democracy. Jimbo la Katanga lina utajiri mkubwa wa madini.
No comments:
Post a Comment