The Greatest Fighter Of All Time, Muhammad Ali amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74. Ali ameiaga dunia huko Phoenix, Arizona baada ya kulazwa hospitali akisumbuliwa na matatizo ya kushindwa kupumua (respiratory complications) na kukohoa. Lakini kwa miaka mingi, Muhammad Ali, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Parkinson aliogunduliwa kuwa nao mwaka 1984 akiwa na miaka 42 na ikiwa ni miaka 3 tu tangu astaafu ngumi za kulipwa mwaka 1981.
Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, msemaji wa familia, Bob Gunnell, amethibitisha kuhusu kifo cha Muhammad Ali kwa kusema, “Baada ya miaka 32 ya kusumbuliwa na ugonjwa wa Parkinson, Muhammad Ali ameiaga dunia akiwa na na miaka 74.
Muhammad Ali alizaliwa Januari 17,1942 (akapewa jina la Cassius Clay) huko Louisville, Kentucky. Alianza masumbwi akiwa na umri wa miaka 12. Mwaka 1960 alielekea Rome, Italy katika mashindano ya Olympics ambapo alishinda medali ya dhahabu. Aliingia katika ngumi za kulipwa muda mfupi baada ya kutoka Rome.
Miongoni mwa mapambano yake yanayokumbukwa sana ni pamoja na lile alilopambana na bondia Sonny Liston ambaye alikuwa anaogopeka sana. Ali alishinda pambano hilo. Pia mapambano dhidi ya Joe Frazier yaliyoitwa Fight Of The Century na Thrilla In Manillayanakumbukwa sana. Kwa upande wa Afrika pambano lililoitwa Rumble In The Jungle la mwaka 1974 mjini Kinshasa dhidi ya George Foreman linakumbukwa sana. Ali alikuwa na miaka 32 tu enzi hizo.
Mbali ya ngumi, Muhammad Ali anakumbukwa kama mtu aliyetetea kwa nguvu zote haki za watu weusi na ukandamizaji wa aina yoyote. Mara baada ya kubadili dini kuwa mwislamu na kuchukua rasmi jina la Muhammad Ali, alikataa kujiunga na jeshi la Marekani mwaka 1967 ili kwenda kupigana katika vita dhidi ya Vietnam. Kitendo cha kukataa kujiunga na jeshi kwenda kupigana kilisababisha anyang’anywe mikanda yote. Hakujali. Na kadiri vita ya Vietnman ilivyozidi kupoteza umaarufu au kutoungwa tena mkono na raia wengi wa Marekani, umaarufu wa Muhammad Ali ulizidi kukua. Katika miaka ya 70s alikuwa miongoni mwa wanamichezo maarufu sana duniani.
Pambano lake la mwisho lilikuwa dhidi ya Trevor Berbick mwaka 1981. Mwaka 1996, kama unakumbuka, Ali ndiye aliyewasha tochi ya mashindano ya Olympic yaliyofanyika jijini Atlanta nchini Marekani.
Atazikwa Louisville, Kentucky alipozaliwa. Pumzika kwa amani #TheGreatest
No comments:
Post a Comment