• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Tuesday, August 7, 2012

Mnyika ‘avalia njuga’ sheria za hifadhi ya jamii

No comments:
 
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika

Gregory Kadendula

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika anakusudia leo kutangaza utaratibu wa kusanya saini za wabunge wasiopungua 10 ili kuunga mkono mpango wake wa kuwasilisha bungeni muswada binafsi wa marekebisho ya sheria za
hifadhi ya jamii ili kurejesha fao la kujitoa linalolalamikiwa nchini kote.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema uamuzi huo umetokana na ushauri wa wabunge wenzake na maoni ya wafanyakazi aliyoyakusanya kwa njia mbalimbali ikiwamo ya mtandao Agosti 4 na 5 mwaka huu.

“Nitaeleza utaratibu wa kukusanya saini za hati ya dharura ya muswada baada ya mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira na majumuisho ya waziri husika,” alisema Mnyika.

Agosti 3, mwaka huu mbunge huyo alieleza kuwa mgogoro uliopo chanzo chake, mbali na marekebisho ya sheria yaliyofanyika Aprili 13, ni
tafsiri potofu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuhusu marekebisho hayo, kuhusu fao la kujitoa.

Alisema tatizo kubwa halikuanzia katika marekebisho ya mwaka huu, bali ni udhaifu wa mfumo wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii ambao unahitaji marekebisho makubwa.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa muswada atakaowasilisha bungeni unahusu fao linalolalamikiwa na mambo mengine ambayo hakuyaweka wazi.

Katika siku za karibuni, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu marekebisho ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii na kufuta kifungu kinachoruhusu fao la kujitoa na kuzua malalamiko kwa wafanyakazi na wanaharakati nchi nzima, kuwa sheria hiyo imelenga kuwanyima haki.

Katika baadhi ya maeneo, hasa migodi imedaiwa kuwa baadhi ya wafanyakazi wameanza kugoma na wengine kuacha kazi baada ya kubaini kuwa hawataweza  kupata fedha zao na mafao kabla ya kufikisha miaka 55 na kustaafu kwa hiyari au miaka 60 ya lazima.


No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ