• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Saturday, September 1, 2012

Dk SLAA AMSHUKIA SITTA

No comments:
 
ADAI NI MNAFIKI, MWONGO,  NI KUTOKANA  NA KAULI YAKE KWAMBA CHADEMA HAKINA VIONGOZI
Waandishi wetu, Iringa
KATIBU Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa amemshukia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta akidai kwamba ni mnafiki, muongo na msaliti na kwamba hafai kuongoza umma wa Watanzania.Dk Slaa alisema hayo katika kikao chake na waandishi wa habari mjini Iringa na kusema amesikitishwa na kauli ya Sitta kwamba Chadema kuna kiongozi mmoja tu; Dk Slaa.
“Nimeamua kuzungumza na nyie kwa vile jana (juzi), wahariri wenu walitaka kujua maoni yangu juu ya kauli aliyoitoa Sitta, akikishutumu Chadema kwamba hakina viongozi na anayestahili kuwa rais bali, ni mimi tu,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Kauli hii inamdhalilisha mwenyekiti wetu na hili linadhihirisha kwamba mtu huyu (Sitta) ni mnafiki, muongo na msaliti....”
Alimtaka Sitta kushughulikia changamoto zinazoikabili CCM ikiwemo kuvunja makundi yanayokimaliza, badala ya kuingilia masuala ya Chadema ambayo alisema hayamhusu.
“Amalize matatizo yanayokihusu chama chake, asituingilie sisi Chadema maana hawezi kutupangia. Sisi tunao utaratibu wetu wa kupata viongozi wetu.”
Alisema CCM kimeshindwa kutatua mambo mengi yanayohusu maslahi ya umma kutokana na kuwa na viongozi ambao ni vigeugeu.
Alimlaumu waziri huyo kwamba alipokuwa Spika wa Bunge, alifunga hoja mbalimbali za kupinga ufisadi zilizowasilishwa na Chadema na kwamba alifanya hivyo kwa maslahi ya kukilinda chama chake. Alisema kwa kufanya hivyo, Sitta hakuwatendea haki Watanzania.
Dk Slaa alizitaja baadhi ya hoja hizo kuwa ni mijadala iliyohusu Mgodi wa Buzwagi, kashfa ya wizi kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa), Meremeta na Richmond, ambayo hadi leo haijawahi kutolewa majibu sahihi licha ya Watanzania kutaka kufahamu ukweli.
Alidai kuwa ukigeugeu wa Sitta unadhihirishwa na ushiriki wake katika kuanzishwa kwa Chama Cha Jamii (CCJ) na kwamba hawezi kukwepa tuhuma hizo kwani aliwahi kuketi meza moja na yeye (Dk Slaa), pamoja na Mbowe kujadili suala hilo.
Sitta hakupatikana jana kujibu tuhuma hizo ikielezwa kwamba alikuwa Burundi kikazi. Hata hivyo, mara kadhaa amekaririwa akikanusha kuhusika na CCJ na amekuwa akidai kuwa hizo ni mbinu za wapinzani wake kisiasa kumpaka matope.
Alidai pia kwamba Sitta siyo mwadilifu kama ambavyo amekuwa akijinasibu, akidai kwamba alipokuwa Spika, alitumia mamilioni ya fedha za Watanzania kujenga Ofisi ya Spika, jimboni kwake Urambo akiamini kwamba, angedumu kwenye kiti hicho milele.
“Kama kweli Sitta ni muungwana, ofisi hiyo anapaswa kuirudisha serikalini au vinginevyo, kila Spika anayeingia madarakani aitumie kwa kuwa hakuna Spika wa Urambo ila wa Watanzania wote,” alisema Dk Slaa.
Kuhusu Mbowe, Dk Slaa alisema Sitta akiwa mwanasheria, hakupaswa kuzungumzia suala la mwenyekiti huyo kuendesha biashara ya kumbi za disko kwa madai kuwa jambo hilo siyo kosa la jinai.
“Serikali imekuwa ikikusanya ushuru kwa sababu kumbi hizo zina vibali na zimesajiliwa na Serikali ya CCM ambayo Sitta amekuwa akiitumikia,” alisema.
Kuhusu Chadema kukosa viongozi wa kuendesha Serikali, Dk Slaa alimtaka Sitta aeleze Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alikopata viongozi waliomsaidia kuiongoza nchi katika kipindi ambacho Tanzania haikuwa na wasomi wa kutosha.
Alisema uongozi si uzoefu, bali maandalizi katika misingi ya uadilifu, uzalendo na weledi, hivyo kauli kwamba Chadema hakina viongozi, haina msingi.
“Ni bora kuwa na viongozi wa kidato cha sita kuliko kuwa na viongozi wasomi wasio na maadili, ikiwa tutaingia madarakani, tutahakikisha sera yetu inatenganisha siasa na watendaji wa Serikali ili kujenga nchi jambo ambalo CCM wameshindwa kwa miaka 50 ya uhuru wa taifa hili,” alisema.

Kuhusu M4C
Katika hatua nyingine Dk slaa alizungumzia kampeni za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) alisema anaishukuru polisi na Serikali kwa kuwa makatibu wenezi wa Chadema.
Alisema Serikali na polisi wanakitangaza chama hicho cha upinzani kwa umma bila kujua kwa kukifuatafuata katika mambo aliyodai kuwa hayana msingi.
Alisema kuwazuia kwao kufanya kampeni za M4C mkoani Iringa kwa sasa, kumezaa matunda kwani wamefanikiwa kuwafikia wakazi wengi zaidi wa Mkoa wa Iringa kutokana na kutembelea zaidi ya mitaa 150 Iringa mjini pekee.
Alisema mfumo huo ndio watakaoendelea kuutumia katika mikoa mingine.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohamed alisema chama hicho hakina udini wala ukabila, huku akiwaasa Waislamu kuacha kutumika kama chombo cha propaganda kuiweka Serikali ya CCM madarakani.
“Ndugu zangu Waislamu jueni Chadema haina udini wala ukabila ila inaongozwa kwa misingi ya katiba. Mnapaswa kufahamu historia ya Chadema na kamwe msikubali kutumika kama chombo cha propaganda,” alisema.
Chadema kinatarajia kufanya mkutano wake mkubwa Jumapili kwenye Viwanja vya Mwembetogwa, Iringa eneo ambalo awali, walizuiwa kufanya mkutano ili kupisha shughuli ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo inamalizika leo.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ