• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Wednesday, March 4, 2015

JE UNAJITAMBUA?

No comments:
 
Je, wewe ni mtu ambaye unafanya jambo halafu baadaye ukija kuulizwa kwa nini umelifanya ukawa na majibu mawili tu; ‘sijui’ au ‘si kina fulani ndo wamefanya’. Basi kuna majina mawili ambayo hawa watu huitwa mtaani, kama si bendera fuata upepo, basi ni boya (huwa linafuata maji yanapokwenda).
Yaani wewe mwenyewe huna sababu binafsi ya kufanya mambo unayofanya zaidi ya kuona wengine wamefanya ukafuata mkumbo tu. Ukiona mtu anafanya mambo dizaini hiyo, huyo hajitambui!
Tuulizane hapa leo kiroho safi tu; hivi unajitambua? Kama unadhani unajitambua endelea kujinoanoa hapa, ila ukiacha kusoma huu mchongo wewe ndo bado hujajitambua kabisa. Ngoja leo tupeane maujanja kuhusu kujitambua.
Binadamu ni viumbe wenye utashi mkubwa unaotupa uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi juu ya maisha yetu ya kila siku. Maamuzi husababisha maisha kusonga mbele au kurudi nyuma. Maamuzi hutokana na tabia. Tabia hujengwa kutokana na fikra na mtazamo ulionao juu ya maisha.
Tabia ni kitu kinachojijenga kwa muda mrefu kutokana na mazingira, jamii inayokuzunguka, mila na desturi, uzoefu maishani na mengineyo. Lakini tabia hutegemea zaidi fikra. Fikra potofu huleta tabia na mtazamo mbovu juu ya maisha.
Kwa ufupi ni kuwa, fikra zako ndio maisha yako. Kubadilisha maisha huanzia kwenye kujenga fikra bora. Njia pekee ya kujenga fikra na mtazamo bora wa maisha yako ni kujitambua.
Kujitambua ni swala la msingi kwa mtu yeyote mwenye nia ya kusonga mbele kimaisha au kubadilisha kabisa muelekeo wa maisha yake. Mafanikio ya kudumu huja baada ya kujitambua.
Kujitambua kunaambatana na mambo mengi ya msingi, yakiwemo – mabadiliko ya fikra, mwenendo, maamuzi na malengo ya maisha.
Kwa mtu yeyote yule, katika umri wowote ule, kujitambua ndio mwanzo wa maisha bora. Huu ndio muda muafaka wa kubadilisha muelekeo wa maisha yako.

Umuhimu wa kujitambua

Kuna faida nyingi sana zinazotokana na kujitambua, chache kati yake ni hizi :

1. Kuishi maisha yaliyo kamili

Kujitambua kunakupa nafasi ya kupanga malengo kutokana na ndoto zako maishani. Malengo ndio msingi wa maendeleo. Tatizo ni kuwa wengi wetutumejawa na hofu, kutojiamini, kuiga, kutojua cha kufanya na kutofahamu umuhimu wa fikra zetu kwenye maisha ya kila siku. Kujitambua kunakupa ujasiri wa kupambana na vikwazo katika safari ya kutimiza ndoto zako.
Kwa ufupi, kujitambua ni mwanzo wa kuishi maisha yaliyo kamili, kifikra na kimtazamo. Unaweza kufanya mambo mengi bila kujitambua, lakini mafanikio yanayodumu hayaji kwa kubahatisha, bali kwa kuelewa njia madhubuti za kufanya mambo ili uweze kufikia malengo. Hii inawezekana kwa kuanza kujitambua.

2. Kutumia kila fursa ipasavyo

Fursa ziko kila sehemu, unachohitaji ni malengo madhubuti unayotaka kutimiza. Una utashi mkubwa na vipaji vingi vinavyoweza kutumika katika kutumia fursa mbalimbali na kuinua maisha yako. Njia pekee ya kuanza kufahamu uwezo wako mkubwa ni kujitambua. Kujitambua ni kufahamu fursa unazotaka kuzitumia kuendeleza maisha kwa kufanya yale  muhimu na kuacha yasiyo na tija kwako.

3. Kujiendeleza zaidi kifikra

Fikra zako zina mchango mkubwa sana katika kuendesha maisha yako. Ili kubadili maisha, ni lazima kubadili fikra. Kubadili fikra ni kitu cha kwanza na cha msingi.
Ili tuweze kufikia malengo, tunatakiwa kupanua wigo wa fikra zetu na kuona mbali zaidi ya leo na kesho. Hii inawezekana kwa kila mmoja wetu, ingawa si kazi rahisi.

4. Kuwa mchango mkubwa kwa jamii

Binafsi naamini – maisha huwa na maana zaidi kama kile unachofanya kitakuwa na mchango mkubwa kwa watu wengi zaidi.
Mtu anayejitambua huwa rasilimali muhimu kwa jamii. Mchango wake huwa chachu ya mabadiliko katika maisha ya wengi. Maendeleo huletwa na watu wenye mtazamo chanya zaidi juu ya malengo yao maishani. Nawe pia unaweza kama ukianza kujitambua.
Kujitambua ni jambo muhimu sana ili kuweza kufanikiwa kwenye maisha yako. Ni chaguo lako – kuchukua nafasi na kuweza kujitambua au kuishi maisha uliyozea na kuendelea kushabikia wale wanaotimiza ndoto zao kila siku.
Karibu kwenye safari ya kujitambua.

Kujitambua ni nini?
Basi hapo warembo mshashika vioo mnajiangalia, sio kujitambua sura, ni deep zaidi.
Ni kufahamu tabia zako, hisia zako, nguvu na udhaifu, jinsi unavyofikiri na kutatua mambo, ambavyo vyote kwa ujumla wake vinatengeneza ‘image’ yako ya jinsi unavyojichukulia na kuwachukulia wengine pia.
Kujitambua hutusaidia kufanya maamuzi sahihi ya jinsi ya kukabiliana na misukumo mbalimbali toka kwa marafiki zetu, ndugu, jamaa na mazingira yanayotuzunguka.
Dalili za upungufu wa kujiamini
Mtu asiyejiamini mara nyingi hushindwa kujitegemea kimaamuzi na kusubiri watu wengine wamuamulie. Hiyo ina maana huna maamuzi binafsi huna msimamo. Hiyo hupelekea kutoheshimika kwenye jamii inayokuzunguka. Na kwa maana hiyo basi hata mahusiano na watu huwa mabovu.
Jinsi ya kujitambua
Kujitambua ni ujuzi. Hii ina maana kuwa unatakiwa kujifunza jinsi ya kujitambua na kufanyia kazi ujuzi huu kila siku ili uweze kuwa mkali wao katika masuala ya kujitambua.
Kwa nini kujitambua ni muhimu?
• Ni tabia ambayo inasaidia kutatua changamoto za kimaisha.
• Kuweza kuelewana na watu.
• Unaweza kujenga mahusiano bora kati yako na familia na marafiki.
• Inasaidia kutatua matatizo ya kimahusianobadala ya kuweka chuki na kinyongo kwa watu, tunaongea nao na kutatua migogoro.
• Moyo unakuwa na amani hata wakati wa matatizo makubwa, kwani unakuwa na uhakika wa jinsi ya kuweza kuyatatua.
• Unafukuzia mbali ‘stress’ zote zisizo kuwa na tija yoyote katika maisha yako.
• Unajijengea kujiamini na uwezo wa kuwapotezea kwa urahisi wale wote ambao wanajaribu kukuletea matatizo katika maisha yako.
Ili kujitambua inatakiwa:
1. Kuwa na maamuzi binafsi. Fanya unachojisikia kufanya pasipo na nia ya kuwaumiza wengine au kuvunja sheria lakini bila ya kufuata mkumbo wa wengine wanachokifanya. Mfano: Kama washkaji zako wanapanga kwenda sehemu, na wewe hujisikii kwenda usilazimishe kwenda na wala usione aibu kuwaambia ukweli.
2. Chukua muda kutafakari kuhusu maisha yako ulipotoka, hapo ulipo na unapotaka kuwa na njia gani zitakusaidia kuwa bora zaidi.
3. Kuwa muwazi katika mambo unayoyafanya.
4. Usipende kuhukumu watu haraka kutokana na vitu wanavyovifanya bila kujua ni nini kilichowasukuma kufanya wanachokifanya.
Kumbuka
Kujitambua ni ujuzi unaoweza kuupata kwa kujifunza na kuutendea kazi. Mtu anayejitambua hufanya maamuzi kwa matakwa binafsi na kwa sababu anazoweza kuzielezea. Jitambue.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ