• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Wednesday, March 4, 2015

Mafanikio yana maana gani kwako ?

No comments:
 
Maisha ni safari ndefu yenye mabonde na milima. Wote tunataka mafanikio maishani, lakini si wote tunaofahamu jinsi ya kufikia mafanikio na kutimiza ndoto zetu. Hivyo, wengi wetu huishi kama bendera kufuata upepo na kushindwa kuamua nini tunataka. Muda wetu maishani hupotea bure bila mafuaa ya msingi.
Je mafanikio ni nini ? Au unawezaje kujua kuwa umefanikiwa ?
Mafanikio ni nini siwezi sema maana ni swala binafsi na kila mtu ana vigezo vyake, lakini nafahamu njia za kuelekea kwenye mafanikio. Mafanikio yanajumuisha vitu vingi sana vidogo vidogo ambavyo vikifanywa kwa ufasaha unaweza kufikia malengo yako.
Ukiachana na kuweza kupata mahitaji muhimu ya chakula, malazi na mavazi, kuna vigezo tofauti nilivoainisha hapa chini.

Kuwa na dira

Mafanikio hupatikana baada ya kuwa na malengo thabiti na kuanza kuyafanyia kazi. Maana asiyejua muelekeo huenda popote kama mwendawazimu.
Maisha bila malengo ni kupoteza muda katika kufanya vitu vingi visivyo na tija. Usipokuwa na malengo maishani utatumika zaidi katika kuwasidia wale waliojiwekea malengo yao. Maisha hayabadiliki kwa mbio za panya bali kwa kuelewa wapi unataka kwenda na kufanya juhudi kufika huko. Hii ndio dira maishani.

Kutimiza wajibu

Kutimiza wajibu ni swala la msingi katika kuleta maendeleo binafsi na jamii. Lakini ni muhimu zaidi kufanya kazi kwa moyo wote na kwa utashi wako wote ili matokeo yake yawe mazuri zaidi.
Watu wanaofanikiwa ni wale wanaojitoa ili kuweza kutimiza kazi zao, majukumu na malengo yao waliyojipangia maishani. Ni watu wanaofanya zaidi ya wanacholipwa kwa sasa ili kuweza kupata zaidi ya wanachostahili hapo baadae.

Kuwa na malengo

Mafanikio huja kwa watu wenye malengo na mipango ya muda mrefu maishani. Hawa ni watu wanaojenga maisha ya baadae sasa. Wanakuwa na ndoto zinazohusisha maisha yao ya miaka 5 hadi 10 ijayo kwa kuanza kuchukua hatua muhimu za kujiendeleza na kufikia huko sasa.

Kuwa na mahusiano bora

Maisha huwa rahisi kama una watu karibu yako. Mafanikio hayana tofauti, ili kufanikiwa unahitaji mahusiano. Hapa umuhimu si bora mahusiano, bali ni mahusiano bora. Yale mahusiano yenye kukujenga na kukukuza kifikra kila siku. Unahitaji watu wenye fikra zinazorandana na zako pamoja na uwezo mkubwa kukuongoza na kukupa mbinu tofauti za kufikia malengo yako.
Mafanikio yanahitaji moyo sababu ni safari ndefu, unapokuwa na mahusiano bora inarahisisha kupata moyo na kufahamu jinsi ya kuruka vihunzi, hasa kipindi mambo yakienda mlama.

Mahitaji ya kiroho

Kila binadamu anahitaji muongozo wa kiroho. Kushiba kiroho ni hatua ambayo humfanya binadamu akue kifikra na kuweza kuwa na matumaini zaidi katika maisha. Hii hali humfanya mtu aweze kupambana na vikwazo akiwa na shauku ya ushindi.
Busara, uelewa na kupevuka akili huanza kwa kufahamu nafasi yako kiroho. Unaweza kufanya mengi bila kukua kiroho, lakini hautoridhika kama utakapochukua hatua ya kukua kiroho.

Mchango kwa jamii

Binadamu wote tunategemeana. Uwe katika hali yeyote ile, una umuhimu wako. Na kila mtu ana nafasi ya kuchangia kwa jamii. Kuishi bila kuwa na faida kwa jamii ni hasara. Binafsi naamini mafanikio ni pale unapoweza kuchangia kuinuka watu wengine zaidi katika safari yako ya mafanikio.
Binafsi naamini kuwa mafanikio ni ile hali ya kuona kuwa maisha yako na  yale uyafanyayo yana mchango mkubwa, si kwa maendeleo yako pekee, bali kwa maendeleo ya watu wengi zaidi.
Kama nilivyogusia kwenye makala iyopita inayosema Je unajitambua, ni kuwa, ukianza safari ya kujitambua, mchango wako utakuwa dhahiri kwa jamii husika. Anza leo kujitambua ili uweze kufikia malengo yako maishani.
Nakutakia safari njema kuelekea kwenye mafanikio ya maishani mwako.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ