• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Monday, August 27, 2012

Chadema yamtaka Nape alipe bilioni 3

No comments:
 


Chadema yamtaka Nape alipe bilioni 3



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimempa siku saba Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aombe radhi na kulipa fidia ya Sh bilioni tatu kwa madai ya kukikashifu chama hicho, la sivyo kitamburuta kortini.

Hatua hiyo ya Chadema inatokana na madai kuwa Nape alikikashifu chama hicho kwa kudai kimekuwa kikiitisha harambee kuwahadaa Watanzania ili kuhalalisha mabilioni ya chama hicho yanayodaiwa kutolewa na wafadhili kutoka mataifa tajiri duniani.
Hata hivyo, pamoja na kupewa siku hizo, Nape ambaye wakati akitoa kauli hiyo Agosti 12, mwaka huu, alidai kuwa anao ushahidi kuhusu kauli yake dhidi ya chama hicho, jana aliliambia gazeti hili kuwa atatoa majibu kuhusu uamuzi wake wa kutakiwa kuomba radhi leo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alidai chama hicho kimeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nape kutokana na madai yake ya uzushi na uongo dhidi ya Chadema.
Alisema Bodi ya Wadhamini wa Chadema iliagiza wanasheria waandike barua ya kumtaka Nape kuomba radhi kwa kutumia njia ile ile aliyotumia kukikashifu chama hicho na kukifitinisha kwa umma wa Watanzania.
“Hii ni pamoja na kuzusha kuwa upo uwezekano wa Chadema kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani,” alidai Mnyika huku akiongeza kuwa tayari kiongozi huyo wa CCM ameshaandikiwa barua ya kisheria tangu Agosti 24, mwaka huu.
Alisema barua hiyo inamtaka aombe radhi na kulipa fidia ya Sh bilioni tatu kwa matamshi hayo aliyodai kuwa ni ya uzushi na uongo yenye maana ya kuwapotosha waliyoyasikia na kuyasoma kuwa Chadema inawalaghai wananchi, kina viongozi wasio waaminifu na kiko tayari kuuza nchi kwa uroho wa madaraka.
“Kipaumbele cha chama chetu katika suala hili ni kuombwa radhi, lakini tumeamua kutaka fidia ya fedha kwa fedheha tuliyopata, ikiwa ni fundisho kuwa uzushi na uongo unagharimu,” alisisitiza Mnyika.
Alisema Agosti 12, mwaka huu baada ya mkutano wa Nape na waandishi wa habari, alimuomba Rais Jakaya Kikwete kueleza Watanzania iwapo propaganda hizo alizoziita chafu zina baraka zake au za chama chake.
“Ukimya wa Rais Kikwete mpaka sasa kuhusu matamshi hayo inaifanya Chadema kuwa na imani yenye shaka kwamba Nape hakutumwa na chama chake kutoa matamshi aliyoyatoa.
“Tunachukua fursa hii kuutaarifu umma kuwa asipotekeleza matakwa hayo ndani ya siku saba, hatua nyingine ni kumfikisha Mahakama Kuu kwa hatua zaidi,” alidai.
Nape kutoa tamko Akizungumza na gazeti hili kuhusu tamko hilo la Chadema, Nape alisema kwa sasa hatozungumzia suala hilo hadi leo ambapo atatoa tamko rasmi kwa upande wake.
Agosti 10, Chadema ilifanya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia mkakati wa kutekeleza operesheni ya vuguvugu la mabadiliko nchini (M4C).
Hata hivyo, Nape katika mkutano wake na waandishi wa habari, aliita hatua hiyo ya Chadema kuwa ni kiinimacho kwa madai kuwa chama hicho kimekuwa kikifadhiliwa mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Aidha, Nape alidai anao ushahidi wa kutosha unaoonesha mabilioni waliyopewa Chadema hivi karibuni na wafadhili kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuendeleza operesheni zao mbalimbali nchini.
Nape katika hilo, alidai kushangazwa na Chadema ambayo badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania kwa jumla wanakopata mabilioni hayo, wanawahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato hayo mtaji wa baadhi ya watu binafsi ndani ya chama hicho.


No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ