• Instagram
  • Twitter
  • Facebook
  • Google+
  • RSS Feed

Monday, August 27, 2012

Yanga yafanya kweli Rwanda

No comments:
 

KOCHA Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet anahofia wachezaji wake wanaweza kuathirika kisaikolojia kama timu itaongeza siku za kubaki Kigali, Rwanda.

Kutokana na hali hiyo amewashauri viongozi wa klabu hiyo timu irejee Dar es Salaam leo kama walivyokuwa wamepanga awali walipoenda Kigali, Rwanda.
Yanga ambao ni mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati walikuwa Kigali, Rwanda kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Bin Kleb akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, alisema hatua ya Yanga kurejea nchini inatokana na ushauri wa Saintfiet.
Alisema kocha huyo amewashauri viongozi wa klabu hiyo kutoongeza siku za kukaa Rwanda na badala yake warudi kuendelea na kambi yao jijini Dar es Salaam na kwamba uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha pamoja juzi usiku.
Alisema katika kikao hicho walimuuliza kocha kama angependa timu hiyo ibaki Kigali au la, na aliwaeleza ni vyema wakarejea Dar es Salaam kwani anahofia wachezaji wangeweza kuathirika kisaikolojia kwa vile walishaeleza wanarudi Dar.
Alieleza kuwa kocha huyo alisema wachezaji waliambiwa awali watarudi Dar es Salaam leo, hivyo suala la kusogeza mbele siku ni kuwatafutia matatizo kwa vile wamekuwa wakiwasiliana na familia zao kwamba wanarudi siku hiyo.
Wakati huo huo, Simba jana iliwapa raha mashabiki wake baada ya kuifunga Mathare United mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.
Simba walikuwa wa kwanza kubisha hodi kwenye lango la Mathare, lakini mshambuliaji kutoka Zambia Felix Sunzu alishindwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Abdallah Juma dakika ya tano ya mchezo huo kwa shuti lake kuokolewa mabeki wa Mathare United.
Dakika ya 17 Simba walifanya shambulizi lingine, lakini Abdallah Juma akiwa na kipa wa Mathare United, Martin Musali, alipiga shuti lililopaa juu ya lango.
Mathare walijibu dakika ya 18 na 25, lakini washambuliaji wake Francis Ouma na Kelvi Omondi walishindwa kuzitumia nafasi hizo. Simba ilipata pigo dakika 30 kwa beki wake kutoka Mali, Komabil Keita kuumia na kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Nyosso.
Mshambuliaji mpya wa Simba raia wa Ghana, Daniel Akufor aliwainua mashabiki wa timu hiyo dakika ya 58 alipofunga bao kwa kichwa kutokana na krosi ya Amir Maftah, lakini dakika tano baadaye Mathare ilisawazisha baada ya Nyosso kujifunga alipokuwa katika harakati za kuokoa.
Simba iliandika bao la pili kwa mkwaju wa penalti mfungaji akiwa Kigi Makasy baada ya Uhuru Selemani kuangushwa eneo la hatari dakika ya 68.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
 
© ALLSTARTZ.BLOGSPOT.COM 2012 - 2017 | ALL RIGHTS RESERVED | CODE + DESIGN BY: DMZ