Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar esSalaam jana akitokea Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.Picha na Fidelis Felix
ALAKIWA DAR KWA KISHINDO, ASEMA NIKO FITI TAYARI KWA KAZI
GREGORY KADENDULA
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka amerejea nchini jana akitokea Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa na kulakiwa na mamia ya watu huku akisema haogopi lolote na yupo tayari kwa kazi.Dk Ulimboka aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 8.15 mchana kwa ndege ya Shirika la South African Airways.
Baada ya kumaliza taratibu zote uwanjani na kutoka nje, Dk Ulimboka alilakiwa na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo madaktari na wanaharakati ambao walijaza karibu eneo kubwa la lango la abiria wanaowasili jambo lililoonekana dhahiri kumsisimua kiasi hadi kufikia kububujikwa wa machozi.
Dk Ulimboka ambaye alipelekwa Afrika Kusini akiwa hawezi kutembea wala kula mwenyewe baada ya Juni 27 mwaka huu kutekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, amerejea akiwa anatembea na mwenye afya njema.
Akizungumza uwanjani hapo, Dk Ulimboka alisema: “Nawashukuru Watanzania kwa kuniombea, nawashukuru madaktari wenzangu, ndugu na jamaa zangu kwa kunisaidia kupata matibabu hadi leo hii narudi nyumbani nikitembea mwenyewe. Hivi sasa niko fiti na niko tayari kwa kazi yoyote.”
Uwanja huo ulikuwa umefurika mamia ya wananchi wakiwemo madaktari ambao walikuwa na shauku ya kumwona Dk Ulimboka, lakini wengi hawakufanikiwa kumwona.
Wingi wa watu ulisababisha kutokea kwa msuguano kati ya madaktari na waandishi wa habari. Wakati wanahabari wakitaka kumwuliza maswali Dk Ulimboka, baadhi ya madaktari walikuwa wakimzuia Dk Ulimboka kujibu maswali licha ya mwenyewe kuonekana kuwa tayari kuulizwa.
Baadhi yao walifikia hatua ya kushika kamera za waandishi huku wengine wakisema... “Mwacheni akapumzike bwana, kwa nini mnamsumbua sumbua.”
Baadhi ya madaktari hao walifikia hatua ya kutumia nguvu dhidi ya wapiga picha wa magazeti na televisheni na hivyo kusababisha vurugu na kelele nyingi katika eneo hilo.
Muda wote wakati Dk Ulimboka akielekea kwenye gari akiwa na maua mkononi aliyokadhibiwa baada ya kuwasili uwanjani hapo, madaktari hao walikuwa wakiimba nyimbo za kuhamasishana ukiwamo Wimbo wa Taifa huku wengine wakisema: “Mtakufa nyie, lakini si Dk Ulimboka.”
Baada ya kupanda gari aina ya Nissan Patrol nyeusi, madaktari hao na wanaharakati na wananchi wengine wakiongozwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananileya Nkya walilisukuma gari hilo hadi katika lango la kutokea katika uwanja huo.
Wanaharakati
Mbali na Nkya, kulikuwa na idadi kubwa ya wanaharakati wengine wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP, Usu Malya.
Wanaharakati hao walikuwa na mabango yaliyoandikwa, “Dk Ulimboka karibu nyumbani uliumizwa kikatili ukitetea afya bora kwa Watanzania.”
Bango jingine lilisomeka: “Dk Ulimboka damu yako ilimwagika na kuamsha ari kwa wananchi kudai za afya.”
Jingine, “Dk Ulimboka wewe ni mpigania haki ya afya bora kwa wananchi wote Mungu na Watanzania wote tuko nawe.”
Malya akizungumza uwanjani hapo alisema kupona kwa Dk Ulimboka na kurejea nchini ni uthibitisho kwamba Mungu amesikia sauti za wanyonge.
“Dk Ulimboka alisimamia haki za madaktari na za Watanzania wote akitaka huduma bora zipatikane kwenye hospitali za umma kwa ajili ya Watanzania wote,” alisema.
Mkurugenzi wa Tamwa, Nkya alisema amefurahi kumpokea Dk Ulimboka akiwa hai kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya wakati akipelekwa kwa matibabu nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema kurejea kwa Dk Ulimboka akiwa amepona kunathibitisha kwamba nchi za wenzetu kuna vifaa vya tiba za kisasa na dawa.
“Kurejea kwa Dk Ulimboka ni mapenzi ya Mungu, huu ni uthibitisho kuwa hapa nchini hakuna vifaa tiba na dawa zinazoweza kusaidia wananchi kama ilivyo kwa wenzetu,” alisema Dk Chitage na kuongeza:
“Madaktari tumefarijika na hii imetupa nguvu licha ya vitisho tunavyopata tutaendelea kupigania haki zetu, haya ni mapambano ya muda mrefu, ”alisema.
Dk Chitage alisema kupona na kurejea nchini kwa Dk Ulimboka ni uthibitisho kuwa watu wengi wasio na uwezo wanapoteza maisha kutokana na kukosekana kwa vifaa tiba na dawa hapa nchini... “Madaktari tupo, lakini tatizo ni vifaa na dawa, hiki ndicho tunachopigania ni haki wananchi kupata huduma za afya nchini.”
Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema kurejea kwa Dk Ulimboka kutasaidia kuwatambua watu waliohusika katika tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa katika Msitu wa Pande.
“Sisi tumefurahi sana, Dk Ulimboka alisimamia haki za madaktari na sekta ya afya kwa ujumla, kurudi kwake kunatupa nguvu ya kuendelea kudai haki za madaktari na wananchi,” alisema.
Dk Ulimboka anarejea nchini huku Serikali na madaktari wakiwa hawajafikia mwafaka kuhusu madai yao.
Madai ya madaktari hao ni hali bora ya mazingira ya utoaji afya nchini, ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa kazini.
Safari ya Dk Ulimboka kwenda kwenye matibabu nchini Afrika Kusini ilitawaliwa na usiri mkubwa alipoondoka nchini Juni 31 mwaka huu, akisindikizwa na Dk Pascal Lugajo na kaka yake, Dk Hobakile Ulimboka na mke wake, Dk Judith Mzovela.
Kutekwa
Dk Ulimboka alitekwa na kufanyiwa vitendi vya ukatili wakati akiratibu mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea na aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya.
Kutokana na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu waliituhumu Serikali kuhusika na tukio hilo, huku Serikali ikikana na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika.
Akisimulia mkasa huo Dk Ulimboka alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Juni 27 katika Klabu ya Leaders, Dar es Salaam alikokuwa na daktari mwenzake na mtu mwingine aliyekuwa amemwita hapo (Leaders).
“Mara, katikati ya maongezi tukaona huyo mtu aliyeniita anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk. Ulimboka). Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini ilikuwa haina namba.”
Wakati Dk Ulimboka alipokuwa akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya Kikwete alisema Serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano baina ya Serikali na madaktari.
Rais Kikwete alisema hayo katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
“Dk Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alichofanyiwa Dk Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama na kinyume kabisa na mila na desturi za Tanzania.
Kauli ya Rais Kikwete kuhusu mgomo wa madaktari inafanana na ile iliyokuwa imetolewa awali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema wanatambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka kuhusu kilichomtokea Dk Ulimboka, lakini ameshangazwa na hisia hizo akisema haoni sababu ya Serikali kufanya hivyo.
Dk Ulimboka alisafirishwa kwenda Afrika Kusini Juni 31, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi baada ya jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia, kueleza mabadiliko ya hali ya afya yake, yaliyosababisha figo kushindwa kufanya kazi.
Ulinzi nyumbani
Nyumbani kwao, eneo la Ubungo Kibangu kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa nje ya nyumba huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Vijana wasiopungua watatu wakiwa wamevaa kawaida walikuwa wamekaa jirani na lango la kuingilia wakiratibu nyendo za wanaopita na wanaotaka kuingia katika nyumba hiyo iliyopo karibu na Shule ya Msingi Ubungo Kibangu.
“Watu walikuwa wengi hapa lakini wametakiwa kuondoka ili kutoa nafasi kwa dokta kupumzika na hakuna ambaye anaruhusiwa kuingia kwa sasa labda kama ni daktari mwenzao,” alisema kijana mmoja anayeishi jirani.
Awali, mama mmoja ambaye alifahamika kama ndugu wa familia hiyo anayeishi karibu na nyumba ya Dk Ulimboka alipoulizwa nyumbani kwa kiongozi huyo wa madaktari alihoji anatafutwa na nani na hata mwandishi walipojitambulisha alimtaka aondoke na kurejea alikotoka.
“Baba wewe nenda nyumbani kwako tu, usitake kujua zaidi,” alisema mama huyo majibu ambayo yalionekana kufanana na ya majirani wengi wa daktari huyo.
No comments:
Post a Comment